1 Corinthians 11

1Nifuateni mimi, kama na mimi ninavyomfuata Kristo. 2Sasa nawasifu kwasababu ya vile mnavyonikumbuka katika mambo yote. Nawasifu kwasababu mmeyashika mapokeo kama nilivyoyaleta kwenu. 3Basi nataka mfahamu ya kuwa Kristo ni kichwa cha kila mwanaume, naye mwanaume ni kichwa cha mwanamke, na ya kuwa Mungu ni kichwa cha Kristo. 4Kila mwanaume aombaye au atoae unabii akiwa amefunika kichwa anakiabisha kichwa chake.

5Lakini kila mwanamke aombae au kutoa unabii hali kichwa chake kikiwa wazi anakiaibisha kichwa chake. Kwa maana ni sawa sawa na kama amenyolewa. 6Ikiwa kama mwanamke hatafunika kichwa chake, na akatwe nywele zake ziwe fupi. Maana ikiwa ni aibu mwanamke kukata nywele zake au kunyolewa, basi afunike kichwa chake.

7Kwani haimpasi mwanamume kufunika kichwa chake, kwa sababu yeye ni mfano na utukufu wa Mungu. Lakini mwanamke ni utukufu wa mwanamume. 8Maana mwanamume hakutokana na mwanamke. Bali mwanamke alitokana na mwanamume.

9Wala mwanamume hakuumbwa kwa ajili ya mwanamke. Bali mwanamke aliumbwa kwa ajili ya mwanamume. 10Hii ndio sababu mwanamke anapaswa kuwa na ishara ya mamlaka juu ya kichwa chake, kwa sababu ya malaika.

11Hata hivyo, katika Bwana, mwanamke hayupo peke yake pasipo mwanamume, au mwanamume pasipo mwanamke. 12Maana kama vile mwanamke alitoka kwa mwanamume, vile vile mwanamume alitoka kwa mwanamke. Na vitu vyote hutoka kwa Mungu.

13Hukumuni wenyewe: Je! ni sahihi mwanamke amuombe Mungu hali kichwa chake kikiwa wazi? 14Je hata asili peke yake haiwafundishi ya kwamba mwanamume akiwa na nywele ndefu ni aibu kwake? 15Je asili haiwafundishi ya kwamba mwanamke akiwa na nywele ndefu ni utukufu kwake? Maana amepewa zile nywele ndefu kama vazi lake. 16Lakini ikiwa mtu yeyote anataka kubishana juu ya hili, sisi hatuna namna nyingine, wala makanisa ya Mungu.

17Katika maagizo yafuatayo, mimi siwasifu. Maana mnapokusanyika, sio kwa faida bali kwa hasara. 18Maana kwanza, nasikia ya kuwa mkutanikapo kanisani, kuna migawanyiko kati yenu, na kwa sehemu ninaamini. 19Kwa maana ni lazima iwepo misuguano kati yenu, ili kwamba wale waliokubaliwa wajulikane kwenu.

20Kwa maana mkutanikapo, mnachokula sio chakula cha Bwana. 21Mnapokula, kila mmoja hula chakula chake mwenyewe kabla wengine hawajala. hata huyu ana njaa, na huyu amelewa. 22Je hamna nyumba za kulia na kunywea? Je mnalidharau kanisa la Mungu na kuwafedhehesha wasio na Kitu? Niseme nini kwenu? Niwasifu? Sitawasifu katika hili!

23Maana nilipokea kutoka kwa Bwana kile ambacho nimewapa ninyi ya kuwa Bwana Yesu, usiku ule aliposalitiwa, alichukua mkate. 24Baada ya kushukuru, aliuvunja na kusema, “Huu ndio mwili wangu, ulio kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa kunikumbuka mimi.”

25Na vivi hivi akachukua kikombe baada ya kula, na kusema, “Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu. Fanyeni hivi mara nyingi kila mywapo, kwa kunikumbuka mimi.” 26Kwa kila muda mlapo mkate huu na kukinywea kikombe, mwaitangaza mauti ya Bwana mpaka atakapokuja.

27Kwa hiyo, kila aulaye mkate au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana. 28Mtu ajihoji mwenyewe kwanza, na hivyo aule mkate, na kukinywea kikombe. 29Maana alaye na kunywa bila kuupambanua mwili, hula na kunywa hukumu yake mwenyewe. 30Hii ndiyo sababu watu wengi kati yenu ni wagonjwa na dhaifu, na baadhi yenu wamekufa.

31Lakini tukijichunguza wenyewe hatutahukumiwa. 32Ila tunapohukumiwa na Bwana, twarudiwa, ili tusije tukahukumiwa pamoja na dunia.

33Kwa hiyo, kaka na dada zangu, mkutanikapo mpate kula, ngojeaneni. Mtu akiwa na njaa, na ale nyumbani kwake, ili kwamba mkutanikapo pamoja isiwe kwa hukumu. Na kuhusu mambo mengine mliyoandika, nitawaelekeza nitakapokuja.

34

Copyright information for SwaULB